Job 12

Hotuba Ya Nne Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Mimi Ni Mtu Wa Kuchekwa

1Ndipo Ayubu akajibu:
2 a“Bila shaka ninyi ndio watu,
nayo hekima itakoma mtakapokufa!

3 bLakini mimi ninao ufahamu kama ninyi;
mimi si duni kwenu.
Ni nani asiyejua mambo haya yote?


4 c“Nimekuwa mtu wa kuchekwa na rafiki zangu,
ingawa nilimwita Mungu naye akanijibu:
mimi ni mtu wa kuchekwa tu,
ingawa ni mwadilifu na nisiye na hatia!

5 dWanadamu wakiwa katika utulivu huwa na dharau kwa wale wenye msiba
kana kwamba ndiyo haki ya wale ambao miguu yao inateleza.

6 eHema za wanyang’anyi hazisumbuliwi,
wale wanaomghadhibisha Mungu wako salama:
wale wamchukuao mungu wao mikononi mwao.


7 f“Lakini ulizeni wanyama, nao watawafundisha,
au ndege wa angani, nao watawaambia;

8 au zungumzeni na dunia, nayo itawafundisha,
au acheni samaki wa baharini wawape taarifa.

9 gNi nani miongoni mwa hawa wote asiyejua
kwamba mkono wa Bwana ndio uliofanya hili?

10 hMkononi mwake kuna uhai wa kila kiumbe,
na pumzi ya wanadamu wote.

11 iJe, sikio haliyajaribu maneno
kama vile ulimi uonjavyo chakula?

12 jJe, hekima haipatikani katikati ya wazee?
Je, maisha marefu hayaleti ufahamu?


13 k“Hekima na nguvu ni vya Mungu;
shauri na ufahamu ni vyake yeye.

14 lKile anachokibomoa hakiwezi kujengeka tena;
mtu aliyefungiwa naye hawezi kufunguliwa.

15 mAkizuia maji, huwa pana ukame;
akiyaachia maji, huharibu nchi.

16 nKwake kuna nguvu na ushindi;
adanganywaye na adanganyaye, wote wawili ni wake.

17 oYeye huwaondoa washauri wakiwa wametekwa nyara,
naye huwapumbaza wanaotoa maamuzi.

18 pHuondoa pingu zilizofungwa na wafalme,
na kuwafunga mishipi ya kiunoni.

19 qHuwaondoa makuhani wakiwa wametekwa nyara,
na kuwaangusha waliojiimarisha muda mrefu.

20 rHunyamazisha midomo ya washauri wanaoaminika,
na kuondoa busara ya wazee.

21 sHuwamwagia dharau wanaoheshimika,
na kuwavua silaha wenye nguvu.

22 tHufunua mambo ya ndani ya gizani,
na kuyaleta nuruni yale yaliyositirika sana.

23 uHuyafanya mataifa yatukuke na kuyaangamiza;
hufanya mataifa kuwa makubwa, naye huyatawanya.

24 Huwaondolea viongozi wa nchi akili zao;
huwapeleka watangetange nyikani pasipo na njia.

25 vHupapasa gizani pasipokuwa na mwanga;
huwafanya wapepesuke kama walevi.

Copyright information for SwhKC